Jumapili, 13 Januari 2019

MAONO- UFUNGUO WA KUFAULU


Sura Ya 2
MAONO – UFUNGUO WA KUFAULU

COMPLIED BY             Rev.Dr. EricK L Mponzi (ThD)      ELAM CHRISTIAN HARVEST SEMINARY TANZANIA
  KWA MAELEZO ZAIDI PIGA SIMU     SIMU 07625332121



Dibaji
    Sasa tumefika mahali muhimu katika kujifunza juu ya kanuni za kufaulu. Tumeelezea na kuchunguza sehemu muhimu ya wakati wetu uliopita na tuko tayari kuanza kutwaa wakati ujao na kuufanya uzae mavuno ambayo Mungu anapenda.
A.   ANZA KWA MAONO
Chunguza mchoro kwenye ukurasa huu. Ni mshale unaoelekea mbele. Unaelekea upande wa wakati ujao.
   Naita mshale huu “njia ya kufaulu” kwa sababu hizi ni hatua ambazo kwazo, kiongozi Mkristo atatumia kufanikisha mapenzi na matakwa ya Mungu.
    Mafanikio yote, malengo yote, taratibu zote – kila kitu anachotaka Mungu ukifanye – ni laazima kianze pale mshale unapoanzia katika mchoro ule. Ni lazima kianze na MAONO.
1.     Bila Maono
Ili kuweza kuelewa vizuri maana niliyo nayo ninapozungumza juu ya maono, kuna haja ya kujadili nini kinachotokea pasipokuwa na maono. Mit 29:18 inafahamika vyema sana katika jamii ya wainjilisti : “Pasipo maono, watu huacha kujizuia [watu huangamia]…”
  Kitu kimoja kwa ujumla hakijafahamika juu ya mstari ule. Maono anayozumgumzia mwandishi wa Mithali sio maono tu ya kuwaleta watu kwa Yesu. Sina ugomvi na matumizi hayo.
    Lakini mwandishi wa Mithali anazungumzia juu ya maono ya kinabii. (Katika Kiebrania neno hilo, “maono” ni neno “chazown” lililomaanisha “ufunuo” au “usia” – yaani, maono). Pasipo na maono ya kinabii watu huangamia.





 (Huacha Kujizuia). Tafsiri moja ninayoipenda imasema, “Pasipo maono watu hukaa bila uangalifu,” yaa wasio na sheria na wasiozuiwa. Wanaishi aina ya maisha yasiyokuwa na kusudi. Hivi ndivyo inavyotokea “mahali pasipo na maono ya kinabii.”
   Kwa mfano: Kwa miaka mingi nchi yangu mwenyewe imepungukiwa na maono na kusudi. Taifa hili limekuwa kama meli isiyokuwa na usukani na matokeo yake, tunakaa ovyo ovyo. Tunachukuliwa bila mwelekeo maalum kupitia kwenye miamba hatari kando kando ya bahari.
     Nilipokuwa mtoto, kulikuwepo na hisia ya maono tuliyoshirikishwa katika shule yetu, ufahamu wa mlengo wa kibinafsi na kitaifa, ufahamu wa kusudi. Leo tunapozungumza juu ya kuwagawia vijana aina hiyo ya maono, wengi katika mamlaka kwenye taasisi ya elimu hutushtaki kwa kuwa wa dini sana tusio na akili.             
    Lakini wakati nilipokuwa mdogo tuliwafundisha watoto wetu aina ya mlengo na kusudi. Tuliisalimu bendera kwa ufahari kila siku, tuliwaheshimu na kuwajali waanzilishi wa taifa, na tulitambua kuwa sisi ni taifa lililozaliwa kuwa huru kwa mataifa mengine. Maneno kwenye Sanamu yetu ya Uhuru yanasomeka “Nitwike uchovu wako, maskini wako, msongamano wa watu wako wanaotamani kupumua kwa uhuru. …”.
     Haikupita miaka mingi tangu tulipoanza kufanya kama watu walioamini kuwa    nchi hii ilikuwa ni bandari ya uhuru. Sasa, tunakaa ovyo ovyo.
2.                               Haja Ya Kuwa Maono Dhahiri.
Sisi ambao ni wahubiri mara kwa mara tunakuwa na mawazo mengi ambayo hayajapangiliwa vizuri. Tunatoka katika malezi ya kitheologia ambayo si dhahiri. Tunajieleza kwa maneno yenye maana isiyo dhahiri au mafumbo yenye ufafanuzi mpana, maana na maelezo ambayo si wazi.
      Mtu fulani akituuliza ni nini lengo letu katika maisha, sisi husema, “Lengo langu ni kumtukuza Mungu.” Je, ni kweli kuwa hili ni jibu la kiroho? Je, ni kweli kuwa ni la ajabu? Ni wangapi wenu mmeng’amua kuwa ni maneno yenye maana hafifu (nyuzinyuzi, isiyo wazi), hasa kwa mtu wa kawaida kule barabarani?
     Jibu la mtu wa wastani anayetembea huko barabarani litakuwa, “Ni nini anachozungumza huyo mpumbavu wa dini?”
     Kama ningaliwauliza ninyi wasomaji kufafanua “kumtukuza Mungu”, kuna maana gani? Bila shaka ningalipata majibu mengi kulingana na idadi ya wasomaji. Hakuna uwazi wa maelezo tukitumia maneno kama hayo.
a.                               Je! Yaweza Kuelezeka?  Ngoja niulize hapa: Wewe unadhani maono yasiyowezekana kuwaelezea wengine yataweza kufaulu?
     Kufanya kazi na kompyuta kumenifundisha kuwa nahitaji kusafisha chumba cha stoo ya akili ya mawazo yangu. Kwa kutokukijali, kimejaa vumbi na utando wa buibui.
     Wakati uliopita sikuzumgumza kwa uwazi. Nilitumia maneno yaliyosika kama ya kiroho lakini mimi mwenyewe pamoja na wengine hatukuyaelewa kabisa. Hii ni kawaida kwa watu wengi wa dini. Tunazungumza kwa namna ambayo watu wengine hawawezi hata kuelewa.
    Kutimiza wito wako, ni lazima kwanza ufafanue maono yako yawe dhahiri ukitumia maneno ya kueleweka, badala ya kutumia changanyiko la maneno ya dini yasiyokuwa dhahiri. Ni lazima uanze na maono yaliyo dhahiri na yaliyofafanuliwa.
b.                               Fahamu Kusudi la Mungu.  Ni sawa kwa maisha yako na kwa huduma yako pia. Sehemu ya mbele ya mshale kwenye mchoro wangu hapo juu ni maono. Kama huna maono yaliyofafanuliwa kwa uwazi utakabiliana na maisha bila kusudi hata kama wengine watafikiri kuwa wewe ni mtu mashuhuri.
     Utapeperushwa na kila upepo kwa sababu hutakuwa na dira, hakuna ramani ya kuendea.  Utakuwa kama Banyani ambaye anajiona kama jani la masika, lililotupwa juu ya ziwa la uzima, likielea ovyo ovyo kila mahali mawimbi yanakolipeleka. Wakristo wengi huishi maisha yao kwa namna hiyo. Hawawezi kutawala zile sehemu za maisha yao ambazo Mungu ameweka katika uwezo wao.
      Lakini Mungu hakupanga kwa namna hiyo.  Anatamani kwamba tujue kusudi lake. Mapenzi yake ni kwamba tuishi maisha kwa mwelekeo, maono, tukijua tunakoenda. Anatutaka tushindane, tukiwa tumedhamiria kupokea taji – kuwa na alama, shabaha, maono ya huko tunakoelekea.
       Hata hivyo, sio tabia ya Mungu kulazimisha maono kwa mtu yeyote. Yesu alisema, “Ombeni nanyi mtapewa.”

B.                              WATU WA MAONO WA BIBLIA
Tuchunguze baadhi ya mifano ya ki-Biblia ya watu wa maono.
1.                               Yusufu
Mwanzo 37:5-11 huelea hadithi ya maono ya Yusufu. Katika umri wa miaka kumi na saba, alipokea maono kwa ajili ya maisha yake katika ndoto mbili Bwana alizompa.
       Kwa urahisi zikisema tu kwamba atakuja kuwa mtawala kati ya watu. Ndugu zake, baba na mama siku moja watakuja kumsujudia na kumtumikia. Haya ni maono ya Mungu kwa Yusufu. Alipowashirikisha maono haya, wazazi wake na ndugu zake waliyakataa.
        Mwanzo 37:10 huelezea, “…Baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota?” ka
tika Mwanzo 37:8, jibu la ngudu zake Yusufu kwa maono yake kwa uwazi lilisema: “…Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.” Baadaye wakafanya shauri juu yake wamwue lakini wakaishia kumwuza utumwani ili kuondokana na “ndoto” zake  na maono yake.
     Ni wangapi wenu mnaamini kwamba maono yatakulete upendo wa papo hapo na heshima? Niamini, si rahisi!
     Kama hadithi ya Yusufu inavyoonyesha, maono  yanaweza kukuingiza katika matatizo makubwa sana. Hata hivyo hadithi yake ilikuwa na mwisho mwenye furaha. Kuna kitu kinachostahili kujifunza hapa, mfano mzuri tunaohitaji kuangalia. Maono kutoka kwa Bwana siku zote hupimwa kwa taabu na mateso.
2.                               Musa
Musa, kama Yusufu , alikuwa na maono. Kuna aya ya kufurahisha katika Matendo 7:22-25 inayoelezea yaliyotokea.
 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo. Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni kwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. Akamwona  mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi Yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu.”
    Mungu alimpa Musa maono, ya kuwa atakuwa mkombozi wa watu wake. Musa alisadiki, akathubutu, akidhani, ndugu zake wataelewa. Lakini, walielewa? Je, walielewa hata kidogo kuliko ndugu zake Yusufu walivyoelewa? Hapana, hawakuelewa! Kweli, Maandiko yanasema, “…hawakufahamu.”
    “Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je, wataka kuniua mimi kama ulivyomwua Yule Mmisri jana?
  Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani…” (Mdo 7:26-29).
     Ukweli kwamba ndugu zake walishindwa kumwelewa, haikumaanisha kuwa maono hayakutoka kwa Bwana, zaidi kuliki katika suala la  Yusufu. Maono yao yalikuwa ya Mungu. Lakini wote wawili, ilikuwa ni lazima kupitia katika muda wa kujaribiwa.
3.                               Ibrahimu
Mfano mgumu sana wa kujaribiwa katika Agano la Kale ni ule wa maono ya Ibrahimu. Mungu alimwambia akamtoe sadaka ya kuteketezwa mwanaye wa pekee Isaka, agizo linaloonekana kupingana na maono ambayo Mungu alikuwa amempa.
      Katika muda huo usiokuwa na matumaini, na Isaka akiwa juu ya madhabahu, Mungu aliingilia kati na kuyafufua maono ya Ibrahimu. Alimrudisha Isaka, na Mungu akatimiza ahadi yake kwa Ibrahimu.
4.                               Paulo
   Paulo alikuwa na maono. Alimwambia Mfalme Agripa,  “…Sikuyaasi yale maono ya mbinguni” (Mdo 26:19). Maono ya Paulo alijulishwa mara tu baada ya kubadilishwa, na maisha yake mara nyingi yalielekezwa, na maono hayo. Sisemi ‘kila mara’ kwa sababu kulikuwepo na tofauti,  na tofauti hiyo ndiyo yenye fundisho la muhimu sana.
     Sasa tunaingia katika somo la majadiliano. Tunaelekea kufikiri kwamba watu wakuu wa Biblia kamwe hawakufanya  makosa. Paulo ni mtu aliyekuwa na madhaifu na tamaa kama tulivyo. Alikabiliwa na matatizo ambayo mimi na wewe tunakabiliana nayo. Hakuwa mtu mwenye uwezo kupita wanadamu wengine au mtakatifu zaidi. Alikuwa na udhaifu wa kibinadamu kama sisi sote tulivyo.
      Kwa sababu ya shauku kubwa ya Paulo ya kuona kuwa Wayahudi wanaongoka, alishindwa kudumu katika mipaka ya maono ya Mungu kwa ajili yake. Ni kule kushindwa kwake kudumu katika mipaka ya maono ya Mungu kwa maisha yake na huduma yake, kulikomfanya kuingia katika matatizo.
     Unafikiri kuwa Paulo hakuwahi kamwe kuingia katika matatizo? Hakika, nafikiri aliingia.
      Matendo 9:15 ni tangazo la maono. Baada ya Paulo kubadilishwa, Bwana akamwambia, “…Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa…”
     Katika Wagalatia 2:7, Paulo aliandika kuwa alikabidhiwa injili ya wasiotahiriwa (watu wa Mataifa). Alikuwa awe mtume kwa watu wa Mataifa na zaidi ya hayo alijua hivyo. Paulo alijua kwa ufasaha maono ya Mungu kwa maisha yake.
    Paulo aliitwa kwa ajili ya watu wa Mataifa, lakini alikuwa ametanguliwa na shughuli nyingine. Je, ni wangapi wenu mnajua shauku yake ilikuwa ni nini? Shauku ya Paulo ilikuwa juu ya ndugu zake Wayahudi.
      Katika Warumi 9:3-4 aliandika “Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwa na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli…”
a.                               Kupokea Katika Maono. Ni dhahiri kwamba, Paulo alikuwa hajaridhika kabisa kuendelea  na maono aliyokuwa amepewa na Mungu kuwaleta watu wa Mataifa kwa Yesu. Kwa hivyo tunakuta tabia ambayo tusingaliweza kuitegemea katika maisha ya mtu kama Paulo.
    Paulo anasema, “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni” (Mdo 20:22). Hapa Paulo yupo Mileto, akiongea na Wazee wa Efeso akiwashirikisha maneno yake ya mwisho kabla hajaondoka.
   Kwa nini Paulo anakwenda Yerusalemu?  Alikuwa anakwenda kwa sababu alitaka kuwaleta Wayahudi kwa Yesu. Alitaka kuwashuhudia Wayahudi, na hivyo anasema, “Basi sasa angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja” (Mdo 20:22-23).
    Kwa nini Roho Mtakatifu humpa ujumbe au humshuhudia mji kwa mji? Je, ni kwa sababu Roho Mtakatifu alitaka kumtesa kwa vifungo na dhiki,  vifungo na minyororo?  Hapana!
     Roho Mtakatifu anapoanza kushuhudia kwa namna hii katika maisha yako, ni ili kwamba uweze kufikiri tena mwelekeo wako. Utafikiria tena  utendaji wako, na mwelekeo na kuokolewa kutokana na mateso yasiyokuwa ya lazima.
    Kila mahali Paulo alikokwenda, Roho Mtakatifu alikuwa akimshuhudia, akisema ya kuwa vifungo na dhiki vilimngoja. Lakini Paulo hakuzuiwa na maonyo hayo. Wala hakuogopa. Alikuwa anakwenda Yerusalemu.
    Paulo alikuwa amejiweka katika njia ambayo hakukubaliana na maono ya Mungu kwa maisha yake. “Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uwezo wa Roho asipande kwenda Yerusalemu.” Na yeye alifahamu nini?  Paulo akaendelea kwenda Yerusalemu!
     Paulo akaendelea mpaka Kaisaria, na nabii fulani aliyeitwa Agabo alimjia. Ni Bwana ndiye aliyemtuma Agabo kwa Paulo ili akae kati ya Mataifa na kufanya Mapenzi ya Mungu kwa maisha yake.
   Agabo atwaa mshipi wa Paulo akajifunga miguu na mikono, akionyesha unabii wake akisema, “…Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa”  (Mdo 21:11). Watu gani? Watu wa Mataifa!
    Paulo alitaka kuwaleta Wayahudi kwa Yesu, lakini maono ambayo Mungu ameanzisha kwa ajili ya maisha ya Paulo yalikuwa ni lazima yatimilike bila kujali kama Paulo anapenda au la. Kama aliendelea kwenda Yerusalemu, wangemfunga mikono na miguu na kumtoa kwa watu wa Mataifa. (Kipaumbele cha kwanza cha maono na wito wake!)  
b.                               Uchunguzi Wa Paulo.  Paulo angeweza kufanya uchaguzi wake. Angeweza kwenda kwa watu wa Mataifa kama mtu huru. Au, angeweza kupuuzia maonyo ya nabii. Kama angepuuza maonyo ya ndugu  waTiro na katika Kaisaria na makanisa ya watu wote wa Mataifa, angelikwenda kwa watu wa Mataifa hali amefungwa minyororo. Je, unajua alichagua nini?
   Paulo alikwenda Yerusalemu!
   Alipokuwa akisali ndani ya hekalu akawa katika hali ya kuzimia roho. Akamwona Yesu akimwambi, “…Hima utoke Yerusalemu upesi, kwa sabasu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu” (Mdo 22:18).
    Kwa hiyo Paulo alifanya nini? Alianza kubishana na Bwana. Alisema kufuatia hilo, “… Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua.” Na Yesu alimjibu, “…Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.”
  Je, Bwana alimwambia Paulo, “Nitakutuma uende kwa Wayahudi?”  Hapana!
   Je, ni kweli ulikuwa ni mpango fulani wa Paulo wa kuwaleta Wayahudi kwa Yesu bila kujali maonyo yote, bila kujali kile ambacho Bwana mwenyewe alimwambia Paulo?
    Ungejisikia kama kupaza sauti masikioni mwa Paulo! Watu wa Mataifa kwa Yesu, Paulo! Watu wa Mataifa kwa Yesu!”
     Je, unajua ni kwa jinsi gani Paulo alivyoondoka Yerusalemu? Kwa minyororo. Je, alitolewa kwa nani? Watu wa Mafaifa!
     Naamini Paulo angaliweza kuishi kwa uhuru zaidi katika maisha yake kama angalidumu  katika mipaka ya maono ya Mungu, kama angalizingatia kazi yake miongoni mwa watu wake, Wayahudi, sana na kuwa na shauku ya kuwaona wameokolewa. Naweza kuwa nimekosea, lakini nafikiri Paulo alikosa kujua mapenzi sahihi ya Mungu hata pamoja na kwamba Mungu alimruhusu kwenda Yerusalemu.
5.                               Dumisha Maono
Maono ni kitu cha muhimu sana, na ni lazima kushikilia maono Mungu anayokupa.
       Tunahitaji kujifunza kutokana na mifano ya Biblia juu ya watu wa maono kama Ibrahimu, Yusufu, Musa na Paulo.
        Kama mtu binafsi (au shirika au chama) akiacha maono Mungu aliyompa, hatimaye atakwenda kukabiliana na aina ya matatizo aliyokabiliana nayo Paulo.
        Mungu anapoanzisha maono kamwe hatabadilisha mawazo yake hata kama watu wangebadilisha mawazo yao. Bwana sio mtu, kwamba atabadilisha mawazo yake. Wala yeye si Mwanadamu hata aweze  kusema uongo.
 Yeye anaposema kitu, hutegemea kifuatwe mpaka mwisho wake! Unaweza kusema “Amina” kwa hilo?
     Maono yanaweza kutimizwa, kama katika hali ya Paulo, bila kujali kwenda nje ya maono. Uchaguzi ni kama tutafuata katika utii na kubakia huru, au tutachukua mwelekeo mwingine wa tofauti na kuishia katika minyororo na kifungo. Uchaguzi ni wetu. Je, utachagua matokeo ya mapenzi yaliyoruhusiwa na Mungu? Au utachagua furaha ya mapenzi yale makamilifu? 
      Dumisha maono na epuka matatizo. Uwe mkweli na mwaminifu kwa maono ya Mungu kwa maisha yako, na utakuwa na mateso kidogo ya kuvumilia.

C.                             MAONO SAHIHI
Tunasimama kidogo hapa kuchunguza baadhi   ya mambo muhimu kuhusu maono sahihi. Narudia tena kusisitiza kuwa maono ni muhimu sana. Bila maono, uongozi hauwezi kutekeleza kitu chochote. Pasipo maono, watu huangamia, watu hutangatanga, watu hukaa bila uangalifu.
1.                               Maono Huanzishwa Ki-Mungu
KWANZA, maono sahihi ni kusudi takatifu la Mungu lililoanzishwa katika moyo wako, katika roho yako. Yanaweza yasije katika ndoto, kama ilivyotokea kwa Yusufu. Yanaweza yasije kama nuru inaying’ara katika barabara ya kwenda Dameski, ikurushe kutoka juu ya punda wako, kama ilivyotokea kwa Paulo.
    Yanaweza yasije kama ilivyotokea kwa Musa. (Biblia haituelezi ni kwa jinsi gani Musa alivyotangulia kujua kwamba atakuwa mkombozi, lakini, kwa namna fulani alifahamu!)
    Maono yake yalikuja kwa upya kwa namna ya kichaka kinachowaka moto bila kuteketea. Miaka arobaini kabla ya wakati huo alijaribu kutekeleza maono hayo katika uwezo wake mwenyewe na alishindwa .
      Yanaweza kuja kama ilivyotokea katika maisha yangu katika maisha ya wengine wengi. Kwa miaka mingi, Mungu, kidogo aliingiza ndani ya roho yangu maono, akinipa uthibitisho usioweza kukwepeka, na kwamba kuna baadhi ya vitu vitakavyotekelezwa kupitia maisha yangu. Nilijua maisha yangu ni lazima yatolewe kuwa wakfu kwa huduma fulani na huduma hizo hazina budi kuzaliwa kutokana na maisha yangu.
       Kwa namna yoyote ile maono yatakavyokuja, ni lazima yatoke kwa Mungu.
2.                               Maono hujaribiwa
PILI, maono hujaribiwa kwa matatizo mengi, misiba mingi. Kwa ujumla yatakuweka katika mgongano na wengine watakaojaribu kukukatisha tamaa na kusema siyo ya Mungu. Kila aina ya hatua itachukuliwa kunyume nawe unapoingia katika maono uliyopewa na Mungu.
   Hivyo ni sehemu ya njia ya Mungu ya kujaribu kila maono. Neno la Bwana hujaribiwa siku zote. Hupimwa siku zote, na sehemu ya njia ya kujaribiwa ni Bwana kuruhusu vipingamizi kuinuka kinyume nawe unapoanza utekelezaji wa maono yake.
3.                               Maono Yana Mipaka
TATU,  tunaweza kubaki katika mipaka au kwenda nje ya mipaka ya maono. Mungu anaweza kutupa maono, lakini baadaye tunaweza kwenda kinyume nayo. Hii ndiyo maana halisi ya “hiari ya nia ya binadamu.” Tunapoona mtu aliyejitoa kwa Kristo kama Paulo, akitoka nje ya mipaka ya maono ya Mungu, sisi tuliobaki tunapaswa kuwa waangalifu. Kumpenda Bwana hakutukingi kutokana na makosa ya juhudi zetu..
4.                               Maono Huatamiwa
NNE, mtu anapokuwa amepokea maono kutoka kwa Bwana – na kujua hivyo – unaonekana kuwepo kwa msukumo wa kuanza kufanya kitu, kuharakisha mambo. Sasa, mara nyingine kunakuwepo mstari mwembamba kati ya juhudi ya Bwana na kutokuvumilia, na naamini kuwa tunahitaji kutembea katika mstari huo kwa uangalifu.
     Paulo Yongi Cho (kutoka Korea) anasema kwamba kutolewa kwa manono ni kama inavyotokea mwungano wa mbegu ya kiume na kike kwa yai la kuku. Baada ya hapo inamlazimu kuku kukaa juu na kuatamia mpaka linapoanguliwa kwenye wonyesho wa uhai.
      Katika hali ya mazoea, anasema Yongi Cho, namna tunvyoatamia maono ni kwa kupitia nyakati za kufunga, maombi na kutafakari. Tunaita katika mawazo yetu maono aliyotupa Mungu na kufikiria juu yautimilifu na uwazi wake mpaka Mungu atakapoanza kudhihirisha undani wake.
 “Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji”
   (Mwa 1:2). Katika lugha ya Kiebrania, neno hilo ‘ikatulia’ (yaani, maana ya neno rachaph ni sawa na kuku juu ya mayai yake) moja kwa moja lina maana “iliatamia”. Mungu aliatamia juu ya uso wa maji.
     Mungu alikuwa na maono kwa ajili ya dunia yake, na yaliletwa na Roho ya Mungu kuatamia juu ya giza lililokuwa juu ya uso wa vilindi. Kutokana na vilindi, ukatokea ulimwengu wenye kuburudisha uliorejesha dunia ili kuwa makazi yanayofaa kwa mtu.
    Je, unayo maono yaliyo wazi? Kama hauna, hebu mngoje Bwana mpaka atakapokupatia moja. Mruhusu akushirikishe maono. Yanakuwa mshale, mwelekeo wa kusudi la Mungu kwa maisha yako. Halafu, yanapokuja, “atamia” juu  yake, yaruhusu yaje katika uhai kwa kuatamiwa
5.                               Maono Ni Lazima Yashirikishwe
“Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji” (Hab 2:2). Bwana anasema,  Iandike njozi [maono].”
     Iandike njozi. Shirikisha wengine. Watu watataka kujua juu ya maono yako. Yanaposhirikishwa kwa wengine, baadhi wataitwa kufanya pamoja nawe. Utaunda kikundi na kwa kikundi, bila shaka, kazi kubwa itaweza kufanyika kuliko ambavyo ungefanya peke yako.
     Ukifanya peke yako, hutaweza kufanya kitu cha maana katika dunia hii. Bali, mtu anayeweza kuwaandaa wengine kutekeleza maono ya pamoja, mtu awezaye kuunda kikundi, anaweza kufanya kazi yenye maana kwa Ufalme wa Bwana.
     Biblia inasema juu ya mmoja kuwafukuza watu elfu na wawili kuwakimbiza elfu kumi. Hiyo ni hatua kubwa! Itakuwaje kwa watatu au wane au hamsini wote wakifanya kazi pamoja katika maono yale yale? Pengine wangewafukuza mamilioni na kujipatia ushindi mkuu katika Jina la Bwana.
   Maono yanayoweza kushirikishwa kwa uwazi ni kitu kinachohitajika sana katika kuwahamasisha watu na fedha kwa kufanikisha kazi ambayo Bwana anataka ifanyike.
     Wakati unapoweza kushirikisha wazi wazi lengo unalokusudia kuliendea, wengi watakuwa tayari na  watataka kukusaidia mpaka utakapolifikia. Rasilmali zitakuja.
     Tatizo siyo la misaada ya kifedha, tatizo ni viongozi ambao hawashirikishi maono na malengo.
     Kutatua tatizo la misaada ya kifedha isiyotosha, yawezekana ni moja ya matatizo marahisi ya uongozi. Kuna fedha nyingi zaidi katika ulimwengu huu kuliko ambavyo watu wanajua ni nini cha kufanyia. Wakati unapoanza kushirikisha maono na malengo, watu watapangana kukusaidia kifedha na katika njia nyingine pia.
    Tatizo la fedha wanalokabiliana nalo viongozi wa kanisa na viongozi wengine wa ki-Kristo hutokea kwa sababu hawajui wanakokwenda.
    Matatizo mengi ya aina tofauti husababishwa na ukosefu wa maono. Wakati kiongozi anapokosa maono, watu hukaa bila uangalifu.
     Kama huna maono, watu hawataki kuchanga kwa kanisa au shirika lako. Itakupasa kushirikisha malengo na mwelekeo wako, na mapango ulio dhahiri unapokwenda kufikia pale unapokwenda. Halafu utapata msaada.
    Nasikia malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa viongozi wa Marekani ambao hawashirikishi maono. Wanasema watu wao wanatuma fedha kwa watu na mashirika yenye huduma kwa njia ya redio na televisheni, “kanisa la umeme” kama inavyoitwa. Unaweza kukisia ni kwa nini? Hakika unaweza.
       Huduma kwa njia ya redio na televisheni zinawashirikisha maono yao, malengo na mipango kupitia “kanisa la umeme”. Wanayo  maono, na watu hujibu.
     Nawaambia viongozi wa kanisa, “Watu wa kanisa lako wasingekuwa wanatuma fedha zao mahali pengine kama mngekuwa mnawashirikisha maono. Wangekuwa wanawasaidia. Kama hujui unakokwenda na wanachama wa kanisa lako hawajui unakokwenda, watakwenda kutuma fedha zao kwa mwingine anayefahamu anakokwenda.”
     Kuna kitu kimoja cha muhimu kukumbuka kama unataka Mungu akupatie msaada kwa ajili ya huduma yako. Ukikosa kitu hiki, unaweza ukawa unashirikisha maono yako na bado hupati msaada wa kifedha.
   Ni nini hiki kitu kingine muhimu? Mungu anatutuka tutumie fedha anazotupa kwa hekima na unyofu (uaminifu). Yeye hataheshimu udanganyifu. Yeye hataendelea hujiahidi kwa kiongozi anayetumia kwa upumbavu au kuishi kiutajiri kwa kutumia matoleo ya sadaka ya watu wa Mungu.
    Kama wewe ni mwanamume au mwanamke wa haki, kama utatumia fedha kwa kile ulichosema zitatumiwa kwazo, bila kuzitawanya, Mungu atashughulika na hitaji lako la kifedha. Mungu humjali mtu ambaye ni mwema, wa haki na uelekevu katika mwenendo wake.  Yeye atamimina kwa wingi zaidi rasilmali ya kutosha kufanya kile alichokuita kufanya. Lakini ni lazima ushirikishe maono, na kuishi maisha yasiyo ya ubinafsi.

Tuombe
  Bwana, Yesu, fafanua kwetu leo, maono uliyo nayo kwa ajili yetu na usimruhusu hata mmoja wetu kuondoka kutoka katika uchaguzi wa maono yako matakatifu. Tuweze kuyakumbatia kwa furaha na mioyo yenye  utayari! Tupe neema tuyakamilishe, na tutakupa wewe shukrani katika Jina la Yesu Kristo AMINI.